UDOM YAWATEMA WANAFUNZI WA TUMAINI

Campus Admin 2018-10-29 20:39:10 Campus News

Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewakataa wanafunzi 138 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JoKUCo) waliokwenda hapo kwa lengo la kuhamia katika chuo hicho kilichopo jijini Dodoma kwa maelezo kwamba hakiwatambui. Chuo cha Josiah Kibira cha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma) kilifikia uamuzi wa kuwahamishia Udom wanafunzi hao kutekeleza agizo la Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) la Septemba 25, baada ya kusitisha utoaji wa mafunzo kwa ngazi zote kwenye vyuo vitano kikiwamo cha Josiah Kibira. TCU ilifikia uamuzi huo na kuvitaka vyuo vilivyofutwa au kusitishiwa kutoa mafunzo, kuwahamisha wanafunzi kwa gharama zao kwenye vyuo vingine. Hata hivyo, mvutano umeibuka baada ya chuo cha Josiah Kibira kuwapeleka wanafunzi 138 Udom Ijumaa iliyopita lakini jana walitimuliwa na uongozi wa chuo hicho kwa kile kilichoelezwa hawatambuliwi. Wakati Udom ikisema haiwatambui wanafunzi hao, Mkuu wa Josiah Kibira, Profesa Wilson Niwavila alisema taratibu zote za kuwahamishia wanafunzi hao Udom zilifanyika kwa makamu mkuu wa Tumaini Makumira kuzungumza na makamu mkuu wa Udom. Kaimu Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Peter Msoffe alisema, “Mimi sijui kuhusu wanafunzi wa Josiah Kibira, mimi niulize kuhusu wanafunzi wa Udom nitakujibu lakini wa chuo kingine sina majibu nao.” Hata hivyo, Profesa Niwavila akizungumzia wanafunzi wake waliotimuliwa Udom, alisema, “Sisi wenyewe hatujui kipi kimetokea, kwani mawasiliano yote yalifanyika ya kuwahamishia hapo na nyaraka zote muhimu za wanafunzi tulizituma.” Alisema jumla ya wanafunzi 160 walipaswa kujiunga na Udom lakini wengine waliomba wenyewe kwenda vyuo vingine. Alisema wanaendelea kufanya mawasiliano na Tumaini Makumira kuhusu suala hilo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo alisema, “Mpaka sasa hao wanafunzi wako chini ya Josiah Kibira na viongozi wa chuo hicho walipaswa kujua wanawapelekaje, taratibu zote zimefuatwa.” Dk Akwilapo alisema uongozi wa Josiah Kibira unapaswa kuwarudisha chuoni, “Makosa ya chuo, hatuwezi kukubali yawaumize wanafunzi.” “Udom hawana tatizo kwani ili mwanafunzi apokewe kuna taratibu zinapaswa kufanywa lakini hao Josiah Kibira hawajazifuta.” Lakini msemaji wa TCU, Edward Mkaku alisema suala la kuwahamisha wanafunzi ni la chuo husika. “Kama Udom haiwataki ndiyo wanapaswa kuieleza TCU kwamba hawa wanafunzi ambao tumeletewa hatuwataki na si mtu mwingine, lakini mpaka sasa hatujapata taarifa hizo,” alisema. Kiongozi wa wanafunzi hao, Job Rojala alisema hali hiyo imewaumiza kwani walielezwa na uongozi wa chuo chao, “Kwamba kila kitu kiko sawa na tunaweza kwenda na ndiyo wakatuleta. “Tumetakiwa tuondoke na baada ya wiki tatu suala letu litaanza kushughulikiwa,” alisema. Mmoja wa wanafunzi aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema walifika Udom, Ijumaa na kuwekwa katika hosteli za chuo hicho. “Lakini jana (juzi) usiku kama saa tatu, tukatangaziwa tunapaswa kuondoka na atakayekaidi atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema. “Ilikuwa tafrani, kwani hatujui tunakwenda wapi, kwa hiyo tukaanza kukusanya mizigo yetu tena na leo (jana) saa 12 asubuhi, tuliondoka na kukaa nje ya Udom ili tusije kamatwa. Viongozi wetu tukiwapigia simu wanatuzungusha, hatuwaelewi,” alisema.