Wabunge wataja changamoto saba za biashara Tanzania

Campus Admin 2019-05-14 20:08:32 Campus News

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ametaja changamoto mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia kushuka kwa Tanzania katika orodha ya nchi zenye mazingira mazuri ya kufanyia biashara. Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Mei 14 2019 na makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis wakati akitoa maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo hayajarejeshwa kwa wahusika na kuchelewa kurejeshwa kwa ushuru wa forodha asilimia 15 katika sukari ya viwandani. Nyingine ni uingizwaji holela wa bidhaa ambazo pia zinazalishwa nchini, kuchelewa kwa taratibu za kupata vibali vya kufanyia kazi nchini na vibali vya Shirika la Viwango Nchini (TBS). Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni hali ya kutokuwa na uzalendo wa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini na upangaji wa kodi. Kanali Khamis amesema kuimarika kwa mazingira ya kufanyia biashara nchini ni moja ya chachu ya kukua kwa sekta ya viwanda na biashara. “Tumeendelea kushuhudia kushuka kwa nafasi ya Tanzania katika orodha ya nchi zenye mazingira mazuri ya kufanyia biashara jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na changamoto mbalimbali zinazolalamikiwa na wafanyabiashara,”amesema. Akifafanua hoja ya upangaji wa kodi, Kanali Khamis amesema kamati hiyo inaishauri Serikali kuwa makini wakati wa kupanga viwango vya kodi kwa kulinganisha na viwango vya kodi duniani hususani ndani ya Jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni wanachama.