Mke wa raisi Ufaransa kurudi darasani

Campus Admin 2019-05-14 20:33:22 Campus News

Mke wa rais wa Ufaransa, Brigitte Macron, ambaye ni mwalimu wa muda mrefu, anatarajia kurudi darasani katika wimbi jipya la vyuo vya mafunzo kwa watu wazima ambalo anajaribu kulitengeneza. Macron, aliyekuwa mwalimu wa lugha ya Kifaransa na tamthiliya hadi mwaka 2015, amekubali kazi ya kusimamia na kufundisha shule mbili zinazojengwa, moja ikiwa katika kitongoji nje ya Paris na nyingine kusini mashariki mwa Ufaransa. Jumatatu, Macron alitembelea shule ya kwanza kati ya shule za "Institut des Vocations", ambayo pia inasaidiwa na nyota wa muziki wa rap, Ben J na mpishi maarufu, Thierry Marx na inapewa fedha na kampuni ya LVMH. Shule hiyo iliyop katika kitongoji kilichotamalaki umaskini kusini mashariki mwa Paris itaanza rasmi mwezi Septemba pamoja na nyingine ambayo majengo yake yako karibu na Valence kusini masharikii mwa Ufaransa, zote zikitoa mafunzo kwa takriban watu 50 wenye umri kati ya miaka 25 na 30 walioacha shule. "Si masomo kama ambayo nilikuwa nafundisha wanafunzi, ni staili ya majadiliano," Macro,n mwenye umri wa miaka 66, ambaye alikuwa akifundisha shule zilizokuwa na sifa nzuri katika mji wa kwao wa Amiens pamoja na Paris, taliwaambia waandishi wa habari. Alisema shule hizo zinalenga kuwapa wanafunzi, ambao watakuwa wakilipia dola 1,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh2.3 milioni za Kitanzania) kwa mwezi, "msingi wa kuwawezesha kuingia kazini". "Tunajua wanahitaji operesheni nne katika hisabati, kujua kuandika Kifaransa, kujieleza na kujenga hoja katika maandishi. Nataka niwape ladha ya fasihi," alisema. Brigitte alikutana na Emmanuel Macron, mwenye miaka 41, wakati akiwa mwanafunzi katika shule aliyokuwa akifundisha mjini Amiens na walianza uhusiano wakati rais huyo akiwa chini ya miaka 20, hali iliyosababisha kashfa ndogo na hasira kwa familia zao. Mama huyo wa watoto watatu alisema kampuni nyingine zimeonyesha nia ya kufuata mfano wa LVMH na kufadhili shule za watu wazima.