Mwanafunzi afariki katika ajali basi la Mtei

Campus Admin 2019-05-15 15:20:16 Campus News

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Silver mjini Babati mkoani Manyara, amefariki dunia baada ya kutokea ajali kati ya basi la Kampuni ya Mtei kugongana na basi dogo aina ya Hiace. Kamanda wa Polisi Mkoani Manyara, Augostino Senga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo asubuhi ya leo Mei 15, 2019 katika eneo la Himiti mjini Babati na kumtaja mwanafunzi aliyefariki kuwa ni Osiligi Paul mwenye umri wa miaka mitatu na miezi mitano. Kamanda Senga amesema ajali hiyo imehusisha basi la Scania Kampuni ya Mtei na basi dogo aina ya Hiace. Amesema mwalimu wa Shule ya Silver ambayo zamani ilikua ikiitwa Deborah, Francis Mollel (36) amejeruhiwa kwenye ajali hiyo pamoja na mwanafunzi Lightness Emmanuel (6) na wakala wa Mtei Paul Shilala (28) wamepata majeraha na wapo Hospitali ya Mrara mjini Babati. Amesema chanzo cha ajali hiyo ni basi la Mtei kuipita gari nyingine bila tahadhari na kugongana na basi dogo kwenye barabara hiyo ya Babati-Kondoa. "Dereva wa basi dogo, Daniel Godfrey (25) naye alijeruhiwa miguuni yupo Hospitali ya Mrara akipatiwa matibabu ila dereva wa basi la Mtei alikimbia na tunamtafuta, amesababisha ajali kwa uzembe wake,’’ amesema Kamanda Senga.